Viongozi
wawili wa Chama cha Mapinduzi (CCM), wanakusudia kumfikisha mahakamani
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda, Jumatatu ijayo kwa madai ya
kuwakashifu, kuwadhalilisha na kuwatukana.
Viongozi
hao ni aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Dar es Salaam, John Guninita
na Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Singida Mgana Msindai.
Akisoma kusudio hilo jana mbele ya waandishi wa habari kwa niaba ya mwenzake, Guninita alisema.
Makonda hakustahili kuteuliwa kushika wadhifa huo kwa kuwa hana maadili ya kuwa kiongozi.
Alisema cheo alichonacho ni cha uyoga ndio maana amekuwa akitukana watu bila sababu za msingi.
“Sifa
ya mtu kuchaguliwa ni lazima awe mnyenyekevu, awe na adabu ya kuzaliwa
na siyo ya photocopy na awe anaheshimu watu hivyo wenye vyeo vya uyoga
hawana sifa hizo,” alisema Guninita.
Alisema
alipofikia Makonda, wameshindwa kumvumilia hali ambayo wametaka haki
zao kuzipata kupitia mahakama kwa kuwa chama kinaendelea kumlinda.
Alisema
hawana ugomvi na Makonda lakini wanamshangaa amekuwa akiwatukana kila
wakati kwa kuwaita ni vibaraka wa CCM na kuwataka waondoke kwenye chama.
Alisema
alishaandikiwa barua na mwanasheria wake, Benjamini Mwakagamba, ya
kumtaka aombe radhi dhidi ya kauli zake na matokeo yake amegoma na
kueleza kuwa alitumwa na chama.
“Waliomshauri
rais kumchagua awe mkuu wa wilaya hawakuwa sahihi na kama ningekuwa
nina uwezo ningetengua hivi ni mtu gani unawatukana viongozi wa dini
halafu leo hii unafanyaje nao kazi,” alihoji.
Guninita
alisema alitegemea kama kuna kosa amelifanya angeitwa na badala ya
kutukanwa na kukashfiwa na kijana huyo ambaye alidai amempita umri na
vyeo.
Alisema
Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) unatumika kuwatukana
viongozi wakati dhana yake ni kuandaliwa kuwa viongozi wenye maadili.
“Huyu
kijana hana maadili ukiachilia mbali kutukashifu alishawahi
kumshambuliwa Jaji Warioba...Alishawahi kumpiga Jaji Warioba eti
alijitetea alikuwa anamlinda. Je huyu Makonda ana mkataba wa kumlinda
jaji Warioba,” alihoji
Guninita
alisema Makonda aliwahi pia kuwatukana viongozi wa dini lakini waliamua
kukaa kimya huku wakimuombea aendelee kuwa na uhai ili wapambane na
Makonda mahakamani.
Alisema Makonda amekuwa akibebwa na kulindwa na viongozi wa CCM wakimtetea, lakini mahakama ni chombo ambacho kitamtenda haki.
Alisema
chama kimefikia sehemu mbaya kuwapo na matabaka ya watu kupewa vyeo
kama uyoga ndiyo maana wanakuwa na jeuri kwa watu. Alisema tabaka hilo
ndilo linalosababisha kuwapo na mgogoro ndani ya chama.
Alisema Jumatatu wataenda mahakamani kuandaa hati ya mashtaka na hivi sasa wanaandaa mchanganuo wa fidia atakayotaka kulipwa.
Alisema
Mwenyekiti wa Chama ambaye ni Rais Jakaya Kikwete anaheshima kubwa ya
kushughulikia migogoro mbalimbali ya nje ya nchi, hivyo wakati umefika
wa kushughulikia migogoro iliyopo ndani ya chama.
Pia
alisema kitendo cha Makonda kuwataka wajiondoe kwenye chama alieleza
kuwa hawatatoka kwa kuwa wamewekeza kwa zaidi ya miaka 40 ndani ya CCM.
Alisema
kama anataka watoke ndani ya chama awalipe fidia la sivyo wao wanauwezo
wa kumlipa fidia kwa miaka mitatu ambayo amekitumikia chama.
Mwanasheria
anayewawakilisha viongozi hao Benjamini Mwakagamba, alisema wateja
wake watafungua kesi Jumatatu dhidi ya Makonda ya udhalilishaji.
Alisema
awali alishaandikiwa barua na kutakiwa kuomba radhi, kuacha
kuwazungumzia viongozi hao pamoja na kulipa fidia ya Sh milioni 100.
Alisema barua hiyo aliijibu na kueleza kuwa alifanya hivyo kwa maelekezo ya chama.
0 comments :
Post a Comment