Kumekuwepo na
utata mkubwa kuhusu
urithi wa mali
za marehemu hasa
inapotokea kuwa marehemu
alikuwa na mke zaidi ya mmoja
na hapohapo watoto
wanaotokana na mama tofauti. Tumeshashuhudia magomvi
makubwa misibani lakini
pia tumeshuhudia na
tunaendelea kushuhudia
utitiri wa mashauri kuhusu
mkanganyiko wa mali za marehemu ambaye familia
yake ni ya watoto
wanatokana na mama
tofauti. Kutokana na hayo
kuna umuhimu mkubwa wa kueleza sheria inasemaje
kuhusu mazingira ya
namna hiyo ili anayemua kuchukua hatua
au kulalamika alalamikie
kitu ambacho ni
haki yake kweli na
anayeamua kuacha aache
akiwa ameridhika kuwa
hajaonewa isipokuwa hicho
alichopata ndiyo haki yake kisheria.
1.NINI MAANA YA MKE
WA NJE YA NDOA.
Mke wa nje
ya ndoa ni
mke ambaye ameishi
na mume kama
mke na mume
lakini akiwa hajafunga
ndoa yoyote ya
kiislamu, ya kanisani, ya serikali au
ya kimila. Ndoa ya kiislamu
hufungwa kwa taratibu za kiislamu
ambazo huhusisha masheikh,
makadhi n.k. Ndoa ya kikiristo
hufungiwa kanisani na
yaweza kufungishwa na
mchungaji, askofu, padre n.k. Ndoa ya
serikali hufungwa katika
mamlaka za serikali kama
kwa mkuu wa wilaya ubalozini n.k.
Na ndoa
za kimila ni ndoa
ambazo hufungwa kutokana
na mila na desturi
za jamii fulani kwa mfano ndoa
za kihaya, ndoa za kichaga n.k.
Kwa hiyo kama mwanamke
hana ndoa yoyote
katika hizi basi yeye
ni mke wa
nje ya ndoa.
2. NINI MAANA YA
MTOTO WA NJE YA
NDOA.
Mtoto wa nje
ya ndoa ni mtoto aliyetokana na
ndoa isiyohalali au mahusiano
yasiyo halali. Hapo juu nimetaja
aina za ndoa halali. Hii ina maana
kuwa iwapo mtoto amepatikana
nje ya ndoa
hizo basi huyo
ndiye anayeitwa mtoto wa nje
ya ndoa.
3. MKE ASIYE NA NDOA
HARITHI.
Kwa mujibu wa sheria
zetu hapa Tanzania
zikiwemo tafsiri mbalimbali
za sheria hizo
ambazo hutolewa na
mahakama kuu pamoja na
mahakama ya rufaa
mke wa wa nje
ya ndoa hutambulika
kama kimada. Neno kimada
sio tusi isipokuwa
ni neno la
kitaalam linalomwakilisha mwanamke
anayeishi na mwanaume
bila ndoa na
ndio maana neno hilihili
limetumiwa na mahakama
katika hukumu zake
mbalimbali.
Kutokana na hilo
ieleweke wazi kuwa
mwanamke asiye wa
ndoa hata
kama anaishi na mwanaume kwa
mtindo ambao ukiungalia utadhani
ni mke na
mume bado ikitokea
mwanaume huyo kufa mwanamke wa
namna hiyo hawezi
kudai chochote katika
mali za yule mwanaume. Mke
halali ni mke ambaye
mahusiano yake na
mwanaume yametokana na
ndoa halali. Nje ya
ndoa halali hakuna
urithi.
Hii isimfanye mtu
yeyote ajisikie vibaya
isipokuwa kinachotakiwa ni
kuhalalisha mahusiano ili
ndoa halali ipatikane.
Aidha ieleweke kuwa
wakati ambao sio wa
kifo kwa
mfano wakati wa kuachana
baina ya mke na
mume ambao wameishi
kama wanandoa lakini
wakiwa hawana ndoa mwanamke
asiye wa ndoa
ana haki ya
kupata mgao wa mali. Na hii ni
ikiwa wameishi wote
kwa zaidi ya miaka
miwili kama mke na
mume na
ikiwa kuna mali
waliyochuma kwa pamoja . Kwa maana
hiyo kwa mazingira
ya kuachana ya kawaida mwanamke asiye
na ndoa anaweza
kudai mali lakini
baada ya kifo
hawezi kudai mali.
4. MTOTO WA
NJE YA NDOA
HARITHI.
Hapo juu nimetaja
aina za ndoa
ambazo hutambuliwa na sheria zetu hapa
nchini. Nikasema kwamba watoto
waliotoka nje ya
ndoa hizo ndio
watoto wa nje ya
ndoa. Ni watoto haohao
ambao hawaruhusiwi kurithi.
Katika kutafsiri sheria hii mahakama
nyingine zimekwenda mbali
kwa kusema kuwa mtoto
wa
nje ya ndoa
haingii katika tafsiri
ya neno mtoto lililo
katika sheria ya
ndoa.
5. KUMHALALISHA MTOTO
WA NJE YA
NDOA.
Sheria inasema kwamba
mtoto aliyezaliwa nje
ya ndoa anaweza kuhalalishwa
kwa kufuata taratibu
za mila na desturi za
jamii husika na
hatimaye kuwa mtoto halali ambaye
anaweza hata kurithi. Kwa
mfano hapa kwetu kila kabila
wanazo taratibu zao katika
kulitekeleza hili. Kwa
kutumia taratibu hizo mtu anaweza kumhalalisha
mtoto wa nje
ya ndoa na
hatimaye akawa na hadhi ya
kurithi .
6. MTOTO WA
NJE YA NDOA
KURITHI IWAPO KUNA WOSIA.
Maelezo niliyotoa hapo
juu kuhusu mtoto wa
nje ya ndoa
kutokurithi yanahusu pale
tu marehemu anapokuwa
hajaacha wosia. Kawaida marehemu
anapokuwa hajaacha wosia familia ya
marehemu au ndugu ndio hushughulika
na kugawana mali za marehemu na
ndipo hapo mtoto wa
nje ya ndoa
hatakuwa na nafasi
ya kurithi. Lakini iwapo
kuna wosia na marehemu
amemtaja mtoto wa
nje ya ndoa
kama mrithi basi
atapewa hiyo mali aliyoamrishwa aipate katika wosia . Hii ndio
sababu kubwa ya
kuhimiza watu kuandika
wosia ili kuondoa utata
wa vitu kama
hivi.
7.USHAURI WA NAMNA
YA KUMSAIDIA MTOTO WAKO KAMA NI
WA NJE
YA NDOA .
Kama unataka mtoto wako uliyempata
nje ya ndoa asipate
taabu baada ya
kufa kwako basi andika
wosia naye umpe
chake. Nje ya wosia mtoto wako
hatopata kitu na wewe waweza
kuwa sababu ya
kumfanya mwanao kuwa mtoto wa mitaani( chokoraa) kwa
kukosa msingi wa kipato.
Nimesema hapo juu
kuwa sheria haina shida
kama mtoto wa nje ya
ndoa amepewa mgao
katika wosia. Lakini nje
ya wosia sheria
inamzuia kupata mali.
MWANDISHI WA MAKALA
HAYA NI MWANASHERIA
NA MSHAURI WA
SHERIA KUPITIA GAZETI
LA SERIKALI LA
HABARI LEO KILA
JUMANNE , GAZETI JAMHURI
KILA JUMANNE NA
GAZETI NIPASHE KILA
JUMATANO.
bashiryakub@ymail.comChanzo; www.fikrapevu.com
0 comments :
Post a Comment