![](https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEi68xY7WzlKroWpCmOn2vStfDGh81ToVHp00bAjWJtnuSxlDSRxzk3TLHhES9-8PEf-_ybZbS6XJUbeXiUtX9EdHwBRNDm4ldNKtvuYDQ-sZe-epm5RStPCJHmlR65PCyhUZWE_zVHtgdk/s1600/pinda2.jpg)
Watendaji
wa Halmashauri waliokaa kwenye vituo vya kazi kwa zaidi ya miaka 10,
wataanza kuhamishwa wakati wowote kuanzia sasa kuleta ufanisi katika
utendaji na kukomesha kufanya kazi kwa mazoea.
Waziri
Mkuu, Mizengo Pinda (pichani) ameagiza ofisi za mikoa ziainishe majina
ya watendaji husika, utaratibu wa kuwahamisha ufanyike kunusuru utendaji
wa kazi kwenye maeneo walikokaa muda mrefu.
Alitoa
agizo hilo juzi wilayani Mufindi katika mkoa wa Iringa. Alisema
serikali imebaini watendaji wanaokaa kwenye vituo vya kazi kwa miaka 10
na zaidi kwenye halmashauri, wanakuwa kikwazo cha utendaji kazi wenye
ufanisi kutokana na kufanya kazi kwa mazoea badala ya kitaalamu.
Alisema, “Niliwahi
kwenda kutembelea halmashauri fulani nikamkuta mzee mmoja amekaa hovyo
kwa kujiachia achia tu na kusahau kuwa ni mtendaji wa serikali. Ilibidi
nimuulize, mzee nawe umo, akasema , ndio mheshimiwa. Nikashangaa, hata
huyu! Kwa jinsi hivi alivyo atafanya kazi vizuri kweli?”
“…Nilipomwuliza
nilipata majibu yaliyodhihirisha kuwa alikuwa alivyo na kutenda kazi
kwa mtindo aliokuwa akiufuata kwa sababu ya mazoea yaliyotokana na
kuwepo kwenye halmashauri husika kwa zaidi ya miaka 10, hii haikubaliki
kwa watendaji wa halmashauri”.
Pinda
alisisitiza, kuwepo kituoni kwa muda mrefu kwa watendaji katika
halmashauri ni miongoni mwa udhaifu unaotoa mwanya wa wizi wa fedha za
halmashauri kwa sababu wanakuwa wakifahamu mbinu za kuiba na jinsi ya
kukwepa kujulikana uhusika.
“Huu
ni ukweli na ushahidi tumeuona katika maeneo ambako watumishi walikuwa
wakiiba fedha. Kuwapangua kulisaidia sana kunusuru fedha zisiibwe katika
baadhi ya halmashauri zilizokuwa na matatizo ya kifedha kutokana na
wizi wakati wa kukusanya kodi na ushuru mbalimbali,” alisema Waziri Mkuu.
Katika
mkutano huo, alimtaka Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza kuandaa
orodha ya watumishi wa mkoa huo waliokaa kwenye nafasi za ajira kwa
zaidi ya miaka 10 na kumpelekea wafanyiwe utaratibu wa kuhamishiwa
vituo vingine.
“Tafuta wote waliokaa zaidi ya miaka 10. Ni lazima tuwabadilishe... niletee orodha mapema iwezekanavyo,” alisema Waziri Mkuu.
Alisema
nia ya mchakato huo ni kuongeza ufanisi kwani watumishi wakikaa sehemu
moja kwa muda mrefu, wanakuwa butu kwa kukosa ubunifu kwenye kazi zao,
wanaota mizizi na kugeuka kuwa chanzo cha matatizo katika baadhi ya
maeneo.
Wakati
huo huo, ameagiza uwekwe uwiano wa idadi ya walimu katika shule zote za
sekondari, kulingana na mahitaji kwa kuhamisha walimu wa ziada kutoka
katika maeneo walipo sasa, kwenda kwenye maeneo yenye upungufu.
Alisema, “Kuna
maeneo nimeona walimu wanakula bwerere tu kwa sababu wako wengi sana.
Hawa inabidi wapunguzwe na kupelekwa kwenye shule zisizo na walimu,
shushu hiyo haihitajiki kwa sababu kuna wengine wanakosa wa
kuwafundisha ilhali wamelundikana eneo moja”.
Jumapili
wakati akizungumza na wakazi wa kata ya Ipogolo, nje kidogo ya mji wa
Iringa, Pinda alimtaka Mkurugenzi wa Manispaa ya Iringa, Ahmed Sawa
kukaa pamoja na Ofisa Elimu wake wapunguze walimu 230 waliozidi mahitaji
kwenye manispaa hiyo, badala yake wawapangie kwenda vijijini.
“Manispaa inahitaji walimu 534 lakini waliopo ni 764. Hapa kuna ziada ya walimu 230 tena kwenye shule za msingi...
"Mkurugenzi kaa na Ofisa Elimu wako muwaondoe walimu waliozidi na kuwapangia waende vijijini ambako kuna mahitaji zaidi,” alisema.
“Kwa
upande wa shule binafsi nako pia tatizo ni lile lile. Walimu wamezidi.
Mahitaji ni walimu 75 waliopo ni walimu 142 ... wanaozidi ni walimu 67,” alisema Waziri Mkuu.
Aliendelea kusema,
“Sina tatizo na walimu wa shule binafsi kwa sababu wao wana mfumo wao
wa ajira lakini hawa wa shule za Serikali ni lazima muwaondoe tena
haraka sana.
"Waondoeni
waende vijijini kwenye mahitaji makubwa sababu ualimu ni ualimu tu,
siyo lazima mtu awe mjini ndiyo afundishe vizuri.”
0 comments :
Post a Comment