MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, amesema hatma yake kisiasa
ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) itajulikana katika
kipindi cha mwezi mmoja kutoka sasa.
Raia Mwema linafahamu kwamba tangazo hilo la kisiasa linahusu
mustakabali wake wa kisiasa ndani ya Chadema, chama ambacho amekitumikia
katika maisha yake yote ya kisiasa tangu akiwa mtoto wa umri wa miaka
16.
Katika mahojiano aliyofanya kwa njia ya mtandao na gazeti maarufu la
Guardian la Uingereza wiki iliyopita, Zitto alisema kuna kitu kikubwa
atakifanya mwishoni mwa mwezi Machi huu.
“Sijawahi kufanya kampeni yoyote kubwa ya kisiasa kupitia mtandao wa
twitter katika maisha yangu ya kisiasa, lakini nataraji kuwa nitafanya
hivyo katika muda wa mwezi mmoja kutoka sasa. Fuatilieni tu twitter na
mtaona,” alisema Zitto pasipo kwenda kwa undani.
Gazeti hilo la Uingereza limeanzisha utaratibu mpya wa kuhoji watu
maarufu kwa kutumia mtandao wa twitter (twit interview) na Zitto alikuwa
mwanasiasa wa kwanza kuhojiwa baada ya kubainika kuwa ndiye anayeongoza
kwa kuwa na wafuasi wengi kwenye mtandao huo hapa nchini.
Akizungumza na gazeti hili kuhusu nini hasa anataraji kukifanya mwishoni
mwa mwezi Machi kama alivyozungumza na gazeti hilo, Zitto alisema ni
mapema kwa sasa kuweka kila kitu hadharani lakini wakati ukifika kila
kitu kitakuwa wazi.
“Niseme kwamba kwenye mahojiano yale nilisema hivyo kweli na
nakuhakikishia kuwa kuna tukio litatokea mwishoni mwa mwezi Machi. Ni
tukio gani na linahusu nini bado mapema kusema.
“Ila naomba kuahidi Watanzania kuwa watafahamu kila kitu kuhusu tukio
hilo wakati ukifika. Hiyo kampeni ambayo itaendeshwa kupitia mtandao wa
twitter na mingineyo, itakuwa ya kisasa na ya uhakika kuliko yoyote
ambayo imewahi kuendeshwa katika historia ya Tanzania, “ alisema.
Zitto alikataa kusema lolote kama tangazo hilo litahusiana moja kwa moja
na kuhama kwake kutoka Chadema kwenda ACT au chama chochote kingine cha
siasa hapa nchini zaidi ya kusema; “subirini”.
Kwa sasa, Zitto ni Mbunge na mwanachama wa Chadema kwa sababu tu ya zuio
ambalo Mahakama Kuu kupitia Jaji John Utamwa liliweka katikati ya mwaka
jana la kufukuzwa kwake ndani ya chama hicho kutokana na kikao cha
Kamati Kuu ya chama hicho.
Zitto na wenzake, Profesa Kitila Mkumbo na Samson Mwigamba, walifukuzwa
na Chadema kwa madai ya kupanga mapinduzi ya kumng’oa madarakani
Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe.
Mwigamba na Kitila wamehamia katika chama kipya cha siasa cha ACT;
Mwigamba akiwa Katibu Mkuu wa muda na mwenzake mshauri na Zitto mwenyewe
amekuwa akihusishwa na chama hicho.
Akizungumzia mahojiano hayo ya Zitto na Guardian, Dk. Kitila Mkumbo
alisema aliyasoma mahojiano hayo lakini akasema anayejua nini kitatokea
mwishoni mwa Machi ni Zitto mwenyewe.
“Mimi kama mshauri wa ACT nasema Zitto kama mwanasiasa makini ana mawazo
yake na mipango yake. Mimi nasisitiza tu kwamba kama ataamua kuja ACT
basi tunamkaribisha kwa mikono yote miwili.
“Tunaamini kwamba yeye ni muumini wa dhana ya Unyerere (Nyerereism)
ambayo ndiyo msingi mkuu wa sera za ACT. Kama ataamua vinginevyo, sisi
pia tutamuunga mkono kwa sababu tunajua itakuwa kwa nia njema,” alisema.
Katika mahojiano hayo na Guardian, Zitto aliulizwa kuhusu masuala
mbalimbali yanayohusu siasa na Tanzania, ikiwamo changamoto za kisiasa,
hifadhi za jamii na nguvu ya mitandao ya kijamii katika siasa za hapa
nchini.
Zitto alisema silaha kubwa ya maendeleo ambayo Tanzania inayo kwa sasa
ni wingi wa vijana ambao alisema kama watawekewa mipango mizuri na
kuwezeshwa kutumika kwa kadri ya uwezo wao, Taifa litapiga hatua kubwa.
Alisema fursa hiyo ina hatari yake nyingine kwamba chini ya asilimia 20
ya Watanzania hawana ulinzi wowote wa Mifuko ya Hifadhi za Jamii, jambo
alilosema ni hatari kwa mustakabali wa Taifa.
Alisema pia kwamba kwa sasa Watanzania wengi wana ufahamu wa masuala ya
mitandao ya kijamii, lakini akasema idadi ya wanaoitumia ni ndogo; huku
akibainisha kuwa baadhi ya viongozi wa juu wa serikali hawako hata
kwenye mitandao kama twitter.
Zitto ana wafuasi zaidi ya 200,000 katika mtandao wa twitter akiwa
anaongoza kwa wafuasi; huku katika nchi nyingine barani Afrika
wanaoongoza wakiwa marais, wanamichezo na wanamuziki maarufu kama Didier
Drogba wa Ivory Coast na Wiz Kid wa Nigeria.
0 comments :
Post a Comment