MBUNGE wa Bariadi Magharibi, Mtemi Andrew Chenge, juzi ameonyesha
utemi wake mbele ya Tume ya Maadili ya Utumishi wa Umma, baada ya kusema
haiwezi kumjadili kwa sababu kuna kesi mahakamani.
Alisema kuna zuio la Mahakama Kuu ambalo limevitaka vyombo vyote vya
Serikali kutojadili suala la miamala ya Akaunti ya Tegeta Escrow hadi
kesi ya msingi itakapoamuliwa.
Tume hiyo inamtuhumu mbunge huyo kuwa alipokuwa Mwanasheria Mkuu wa
Serikali, alitumia madaraka yake vibaya katika uuzaji wa hisa za Kampuni
ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) kwenda Kampuni ya VIP
Engineering Tanzania Limited.
Itakumbukwa wakati suala la Tegeta Escrow likijadiliwa bungeni, Chenge
alidaiwa kupewa sh bilioni 16 na mmiliki wa VIP Engineering Tanzania
Limited, James Rugemalira.
Jana, kabla ya Chenge kuieleza Tume ya Maadili kuwa haiwezi kumuhoji,
Mwanasheria wa tume hiyo, Hassan Mayunga, alisoma mashtaka
yanayomkabili.
“Mlalamikiwa akiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, mwaka 1995 aliishauri
Serikali kuingia mkataba wa miaka 20 wa kuongeza uzalishaji wa umeme na
Kampuni ya IPTL.
“Mlalamikiwa baada ya kustaafu wadhifa wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali
Desemba 24, mwaka 2005, mwaka 2006 aliingia mkataba wa kuwa Mshauri
Mwelekezi wa Kampuni ya VIP Engineering Tanzania Limited iliyokuwa na
hisa asilimia 30 kwenye Kampuni ya IPTL.
“Kitendo cha kuingia mkataba na Kampuni ya VIP ni ukiukwaji wa kifungu
cha 6(i) cha sheria ya maadili ya viongozi wa umma ambayo inamzuia
kiongozi wa umma kujinufaisha katika utumishi wake uliopita kwa kutumia
taarifa alizozipata wakati alipokuwa akitekeleza majukumu yake kwa
masilahi binafsi,” alisema Mayunga.
Alisema kitendo cha mlalamikiwa kuendelea kuwa mshauri wa Kampuni ya VIP
huku akiwa na wadhifa wa ubunge, ni ukiukwaji wa kifungu cha 6(e) cha
sheria ya maadili ya viongozi wa umma ambayo inamzuia kiongozi wa umma
kujiingiza katika mgogoro wa kimasilahi.
Mayunga alisema mkataba ambao mlalamikiwa aliingia na VIP, ulimpatia
masilahi ya kifedha ya Sh bilioni 1.6 kinyume na kifungu cha 12(1)(e)
cha sheria ya maadili ya viongozi wa umma.
“Mwaka 2014 mlalamikiwa aliingiziwa fedha kiasi cha Sh bilioni 1.6 na
kampuni hiyo katika Benki ya Mkombozi wakati hakutamka mapema kama
aliwahi kuwa mwanasheria mkuu wa Serikali na kwamba ana masilahi binafsi
na kampuni hiyo wakati alikuwa akijua kuwa Shirika la Umeme (Tanesco)
lina mgogoro na IPTL,” alisema.
Chenge
Baada ya kusomewa mashtaka, Chenge aliyakana na kuomba mwongozo kwa
madai kuwa suala hilo lina zuio la Mahakama Kuu, hivyo basi tume hiyo
haiwezi kujadili suala hilo hadi kesi ya msingi itakapokwisha.
“Napata shida kujadili suala hili, mimi nikiwa kama mwanasheria
linanisumbua kidogo, kutokana na umahiri wako jaji, ninaomba upitie zuio
lililotolewa na Mahakama Kuu kwa kina ili uweze kuangalia kisheria, je
inaruhusiwa kujadili au la,” alisema Chenge.
Baada ya majadiliano hayo, Mwanasheria Mayunga alisema amri ya mahakama
haihusiani na kazi za baraza kwani katika oda ya mahakama, hakuna
kipengele cha kuzuia kujadili suala hilo.
“Ibara ya 132 ya sheria ya mwaka 1987, ibara ndogo ya kwanza ambayo
inaeleza kuwa kutakuwa na sekretarieti ya maadili ya utumishi wa umma ya
kuchunguza mienendo ya viongozi na watumishi wa umma.
“Taasisi hii ni huru na kwamba inafanya kazi endapo kuna taarifa ya
ukiukwaji wa maadili kwa viongozi katika suala la rushwa au kutumia
madaraka yao vibaya,” alisema Mayunga.
Baada ya kusema hayo, Mwenyekiti wa barza hilo, Jaji Mstaafu Hamis
Msumi, alihairisha shauri hilo na kusema watapitia zuio la mahakama hiyo
ili waweze kuangalia kama ni kweli linaweza kuwazuia kufanya kazi zao
au la na leo waweze kutoa uamuzi.
“Tumeomba muda kidogo ili tuweze kuipitia hii oda ya mahakama na
kuiangalia kwa umakini kama ni kweli inatuzuia tusijadili suala hili au
la, leo tutatoa uamuzi kamili,” alisema Jaji Msumi.
Aliongeza kutokana na hali hiyo, baraza hilo linapitia hoja ya
mlalamikiwa na mlalamikaji ili kuangalia mambo ya kisheria yanayohusu
kujadili au kutokujadili suala hilo.
Chenge akiwa nje ya Ukumbi wa Karimjee ambako mashauri hayo
yanasikilizwa, waandishi walitaka kusikia maoni yake juu ya suala hilo
na yeye akawajibu: “Andikeni kama mlivyoona na kusikia.”
Mbunge huyo alifika katika viwanja vya Karimjee saa 3:00 asubuhi kabla
ya kuanza kusikilizwa kwa shauri lake saa 3:15 baada ya jopo la majaji
na mwenyekiti wa baraza hilo kuwasili.
Baraza hilo pamoja na kutolea uamuzi wa shauri la Chenge wa kusikilizwa
au kutosikilizwa leo, pia linatarajia kumuhoji Mbunge wa Muleba Kusini,
Profesa Anna Tibaijuka kwa siku mbili – leo na kesho.
KASHFA ZA CHENGE
Chenge ametajwa kuhusika katika kashfa mbalimbali, zikiwamo za rada,
ajali iliyoua watu wawili na uchotwaji fedha katika akaunti ya Tegeta
Escrow.
Rada
Chenge alitajwa katika kashfa ya ununuzi wa rada, ambayo ilimlazimu kuachia uwaziri.
Rada hiyo ilinunuliwa kutoka Kampuni ya BAE System ya Uingereza kwa dola
milioni 40 mwaka 2001, kiwango kilicholistua Bunge la Uingereza.
Katika uchunguzi wa suala hilo, ilibainika kuwa Chenge alikuwa na
akaunti kwenye Kisiwa cha Jersey iliyokuwa na zaidi ya dola milioni 1
(sawa na zaidi ya Sh bilioni 1.8) hali iliyofanya ashinikizwe kujiuzulu
wadhifa wake wa uwaziri wa miundombinu.
Ajali iliyoua wawili
Wakati kashfa ya rada ikiendelea, Chenge alihusika katika ajali iliyoua wanawake wawili mmoja akitajwa kuwa mtu wake wa karibu.
Baada ya ajali hiyo, alishtakiwa kwa makosa ya kuendesha gari kizembe na bila kuwa na bima.
Alihukumiwa kwenda jela miaka mitatu au kulipa faini ya Sh 700,000 ambazo alilipa.
Tegeta Escrow
Mwaka jana alijikuta kwenye kashfa ya uchotwaji wa zaidi ya Sh bilioni
300 kwenye akaunti ya Tegeta Escrow, ambapo alidaiwa kuchotewa Sh
bilioni 1.6.
KAULI TATA
1. Alipopata kashfa ya kuchota Sh bilioni 1.8 za rada, alisema ‘Ni vijisenti’.
2. Alipopata kashfa ya kuchota Sh bilioni 1.6 za Escrow, alikuja na
kauli mbili: “Mimi ni tumbili, hata kwenye hii (kashfa ya Escrow)” na
“Mimi ni nyoka wa makengeza, nawatafutia wananchi fedha.”
3. Wakati wa kelele za kumtaka Chenge na wenzake kujivua gamba, mbunge huyo alisema: “Gamba limevuka limeishia kiunoni”.
4.Ashauri waliohusika na kashfa ya Escrow, mamlaka ya uteuzi (Rais)
iwashughulikie na wapinzani wakaungana naye, lakini CCM wakagoma.
NYADHIFA ALIZOWAHI KUSHIKA
2014: Mwenyekiti wa Kamati ya Uandishi wa Katiba Mpya.
2006/15: Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti.
2006/08: Waziri wa Miundombinu.
2006: Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
1993-05: Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
1991-93: Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
1972-73: Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Aliwahi pia kuwa Mwenyekiti wa Kamati Ndogo ya Maadili ya CCM.
0 comments :
Post a Comment