Home » » Rais Kikwete atoa Salamu za Rambirambi kufuatia kifo cha Mbunge wa Mbinga,Mh. John Komba

Rais Kikwete atoa Salamu za Rambirambi kufuatia kifo cha Mbunge wa Mbinga,Mh. John Komba

Written By MWAYANGASPORTS on Sunday, 1 March 2015 | 04:46

 
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amepokea kwa mshtuko mkubwa na huzuni nyingi taarifa za kifo cha ghafla cha Mheshimiwa Kepteni John Damian Komba, Mbunge wa Jimbo la Nyasa, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya taifa ya CCM na msanii hodari sana wa kizazi chake.

Katika salamu zake za rambirambi kwa Spika wa Bunge, Mheshimiwa Anne Semamba Makinda na Katibu Mkuu wa CCM, Mheshimiwa Abdulrahman Kinana, Mheshimiwa Kikwete amesema:   
   “Nimepokea kwa mshtuko mkubwa na huzuni nyingi taarifa za kifo cha ghafla cha Mheshimiwa Kepteni John Komba, ambacho nimejulishwa kuwa kimetokea mchana wa leo, Jumamosi, Februari 28, 2015, kwenye Hospitali ya TMJ, Dar es Salaam.”

Kwa hakika, sina maneno ya kutosha kuelezea kwa fasaha hasara ambayo taifa letu na chama chetu kimepata kutokana na kifo cha Kepteni Komba. Taifa letu limepoteza hazina kubwa na mtu muhimu. 
 Nimejua Kepteni Komba kwa muda mrefu sana, nimefanya naye kazi. Alikuwa msanii ambaye kiwango chake cha usanii kilikuwa hakipimiki, alikuwa na sifa kubwa za uongozi, alikuwa mpenzi, mzalendo na mtu mwaminifu sana kwa taifa lake na katika jambo lolote aliloliamini.,”
"Ndani ya Chama chetu, naomba salamu zangu ziwafikie wanachama wetu wote kwa kupoteza mwanachama mwenzao, ziwafikie viongozi na hasa wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ambayo imepoteza mwakilishi mwenzao na wasanii wote wa Tanzania One Theatre (TOT) ambao Kiongozi wao ameondoka duniani,”
 
Naungana na wanafamilia kuomboleza kifo cha rafiki yetu, ndugu yetu na kiongozi mwenzetu. Napenda wanafamilia wajue kuwa natambua uchungu wao katika kipindi hiki na tahayari yao ya  kuondokewa na mhimili wa familia.  
 
"Niko nao katika maombolezo na katika kumwomba Mwenyeji Mungu aiweke peponi roho ya Marehemu Kepteni John Damian Komba. Amen.”

SHARE

About MWAYANGASPORTS

0 comments :

Post a Comment