Home » » Watoto wa vigogo marufuku kupewa vizimba Mwanjelwa

Watoto wa vigogo marufuku kupewa vizimba Mwanjelwa

Written By MWAYANGASPORTS on Friday, 27 February 2015 | 03:45

 
WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda amepiga marufuku watoto wa vigogo wa serikali, mashirika binafsi, taasisi , madiwani na wanasiasa wengine kupewa vizimba vya biashara katika soko kuu la kisasa la Mwanjelwa mkoani humu, kuruhusu waliounguliwa bidhaa kwenye soko la awali wapate nafasi.
 
Akihutubia maelfu ya wananchi katika eneo la soko hilo kwenye halmashauri ya Mbeya Mjini, baada ya kuweka jiwe la msingi, Waziri Pinda alisema, jengo la soko hilo kubwa la kisasa litawafaa hata wafanyabiashara wadogo wenye ulemavu wa viungo.
 
Alisema litawafaa kwa sababu amelikagua na kuona lina miundombinu inayowajali kuanzia kwenye ngazi, lifti hadi vyooni, hivyo, visitokee visingizio wakanyimwa vizimba kwa madai ya kutoweza kupanda na kushuka kwenye soko hilo, na sababu nyingine zisizo na mashiko.
 
“Ninaonya mapema kuwa soko hili ni kwa ajili ya wajasiriamali wadogo ambao ndio waliounguliwa na soko wakati ule ilipotokea ajali ya moto na kupata hasara kubwa kutokana na bidhaa zao kuteketea...”
 
“Itakuwa dhambi kama wataacha kupewa kipaumbele wakati wa ugawaji wa vizimba hivi, kwa sababu wao ndio hasa wanaostahili, ndipo kama itatokea kuwa nafasi zinabaki, zigawiwe kwa wajasiriamali wadogo wengine kulingana na maombi yao,” Pinda alisema.
 
Aliongeza kuwa hategemei kuona watoto kama wa akina Mizengo Pinda, madiwani, wanasiasa na watoto wa vigogo wengine wa serikali, taasisi na mashirika wakipewa nafasi kwenye soko hilo.
 
Aliwataka wafanyabiashara ndogo watakaopewa vizimba katika soko hilo, wasiviuze kwa tamaa, bali watafute mitaji kuanzia sasa, ili wasishindwe kuvitumia wakati litakapoanza kufanya kazi.
 
Kwa mujibu wa Kaimu Mkuu wa Mkoa huu, Deodatus Kinawilo soko hilo lililojengwa kwenye eneo la ukubwa wa ekari 4.7, kwa zaidi ya Sh bilioni 13, zilizokopeshwa na benki ya CRDB, linatarajiwa kuanza kazi Aprili mwaka huu.
 
Hata hivyo, kutokana na jinsi alivyoona maendeleo ya ujenzi huo na hatua iliyofikiwa na mkandarasi wa ujenzi huo ambaye ni kampuni ya ujenzi iitwayo Nandra Engineering Construction, Waziri Mkuu alisema yeye anatoa hadi Juni mwaka huu, wafanyabiashara wadogo wawe wamekwisha ngia na kuanza kufanya biashara.
 
Pia, alikumbushia umuhimu wa kulipa kodi ya serikali na kusema kuwa ndio itakayosaidia soko hilo lidumu kwa sababu fedha za kodi zinazokusanywa kutoka kwa wafanyabiashara mbalimbali zinatumika kuboresha miundombinu katika maeneo mbalimbali ya jiji hilo, zikiwemo barabara kuu zitakazowasafirisha wanunuzi kutoka maeneo tofauti ya ndani na nje ya Tanzania.
 
Wakieleza ni kwanini ujenzi wa soko hilo haukukamilika kwa wakati kama ilivyotakiwa awali, Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya, Mussa Zungiza na Meya wa Jiji , Athanas Kapunga walimweleza Waziri Mkuu kuwa ni kwa sababu ya mgogoro uliotokea kati yao na mkandarasi aliyekuwa akijenga mwanzoni, kufuatia kumkatishia mkataba wa ujenzi.
 
Katika hatua nyingine, mke wa Waziri Mkuu, Tunu Pinda, aliwashawishi wanawake wajiunge katika makundi kuanzisha biashara kubwa katika soko hilo, itakayowainua kiuchumi.

SHARE

About MWAYANGASPORTS

0 comments :

Post a Comment